Monday, 25 March 2013

FAIDA ZA MTI WA MBUYU


MBUYU: MTI WENYE FAIDA LUKUKI KIAFYAMungu ameumba miti na mimia kwa ajili ya binadamu. Kila mti au mmea una makusudio yake. Mbuyu ni miongoni mwa miti yenye faida nyingi na maajabu mengi. Vitu vyote vilivyomo kwenye mbuyu vinatumika kama chakula au dawa kwa faida ya binadamu.

UBUYU WENYEWE
Unga wa ubuyu unaelezwa kuwa na vitamini na madini mengi kuliko matunda mengine. Inaelezwa kuwa unga wa ubuyu una Vitamin C nyingi kuliko hata machungwa na ina kiwango kingi cha madini ya kashiamu (Calcium) kuliko hata maziwa ya ng’ombe.
Aidha, unga wa ubuyu ni chanzo kikubwa cha madini mengine aina ya chuma (iron), Potasiamu (Pottasium) na manganizi (magnesium). Inaelezwa kuwa kiwangao cha Potasiamu kilichomo kwenye unga wa ubuyu ni mara sita zaidi ya kile kinachopatikana kwenye ndizi. Ubuyu ni muhimu sana kwa watu wenye matatizo ya figo.
Vile vile unga wa ubuyu una uwezo mkubwa wa kuongeza kinga ya mwili  (antioxidant) kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha virutubisho vya kuongeza kinga mwilini dhidi ya magonjwa nyemelezi. Kiwango chake kinazidi hata kile kinachotolewa na matunda mengine kama vile Krenberi, bluberi na blakberi. Ili upate faida za unga wa ubuyu zinazoelezwa hapa, lazima ule ubuyu halisi usiochanganywa na kitu kingine cha kuongeza ladha.

MAFUTA YA UBUYU
Mafuta ya ubuyu, ambayo hutengenezwa kutokana na mbegu zake, ni mazuri kwa kulainisha ngozi na kukarabati au kuponya ngozi iliyoathiriwa na magonjwa ya ngozi mbalimbali, ikiwemo fangasi, vipele na chunusi.
Mafuta ya ubuyu yana uwezo wa kuifanya ngozi kuwa nyororo na laini kutokana na kuwa na kiasi kingi cha mafuta aina ya Omega 3 na Omega 6 na ina kiasi kingi cha Vitamin A, D na E ambazo zote ni muhimu kwa ustawi na uimarishaji wa ngozi ya binadamu.
Mafuta ya ubuyu yanaelezwa kuwa na virutubisho vinavyoweza kuondoa mikunjo ya ngozi, mabaka, michirizi na hata makunyazi na kuicha ngozi kuwa mpya. Hutoa kinga dhidi ya uharibifu wowote wa ngozi unaoweza kujitokeza baadaye.

JINSI YA KUTUMIA MAFUTA
Mafuta ya ubuyu unaweza kuyatumia kwa kupaka usoni au mwili mzima moja kwa moja. Unaweza kuyatumia mafuta haya kwa kupaka sehemu tu iliyoathiriwa kama dawa. Unaweza pia kuchanganya na mafuta au losheni unayotumia.
Ili kupata matokeo unayotarajia, hakikisha unatumia mafuta halisi ya ubuyu ambayo hayajachanganywa na kitu kingine wakati wa kutengeneza.

UPATIKANAJI WAKE
Bidhaa za ubuyu zimeanza kujipatia umaarufu nchini Tanzania na hivi sasa kuna makampuni na wajasiriamali binafsi wanaojishughulisha na utengenezaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na ubuyu, hivyo upatikanaji wake ni rahisi iwapo utaulizia maeneo unayoishi.
Bidhaa zingine zinazoweza kutengenezwa kutokana na mti huu ni pamoja na majani yake ambayo hutumika kama dawa, mizizi na magamba yake pia. Kwa ujumla mti wote wa ubuyu una faida na hakuna kitu kinachotupwa kwenye mti huu ambao ni miongoni mwa miti yenye matunda bora yaliyopewa jina la ‘superfruit’.

No comments:

Post a Comment